Serikali imesema wanafunzi 700 watakaofaulu vizuri masomo ya sayansi na wakihitaji kusoma vyuo vya hapa nchini, watasomeshwa bure.
Aidha, wanafunzi watakaosoma masomo ya sayansi, uhandisi, Tehama, elimu tiba na hisabati hawatakuwa na gharama za kulipia, kwamba serikali itawagharamia kila kitu.
Hayo yalisemwa juzi na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda wakati akizindua maadhimisho ya elimu, ujuzi na ubunifu yaliyofanyika kitaifa katika Mkoa wa Tanga.
“Siyo mikopo, serikali itakulipia gharama zote ikiwamo kujikimu, malazi na chakula mpaka umalize kusoma, ili mradi waendelee kufanya vizuri kwenye masomo yao kwenye vyuo wanavyosomea,” alisema Prof. Mkenda.
Soma Zaidi:ElimuYa Ukwamuaji Wa Urasimishaji Wa Ardhi
Vilevile alisema kupitia ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeelekeza kuendeleza sayansi na teknolojia na Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza zitengwe fedha kwa ajili ya kuwasomesha vijana wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Alisema serikali iko katika mchakato wa kujenga shule 100 za mafunzo ya amali kwa nyanja ya ufundi kwa nchi nzima, ili kuwawezesha vijana wa kitanzania kujiajiri au kuajiriwa kupitia ujuzi watakaopata kwenye vyuo hivyo.
Kadhalika, Prof. Mkenda amezindua rasmi mwongozo wa Samia Scholarship, kwenda kusomea elimu ya juu ya nyuklia nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuongeza madirisha ya wanaotaka kwenda kusomea.
Licha ya kuzungumza hayo, alisema maonesho hayo ni chachu ya maendeleo kwa sekta ya elimu katika ubunifu na kusisitiza kuwa wenye ubunifu wajipange na kuwania fursa iliziko kwenye maadhimisho hayo.
Alisema: “Watu wote wenye ubunifu wajipange na wakae tayari kwa kuwa maonesho haya yatafanyika kila mwaka, pia yatafanyika walau kwa miaka miatatu katika mkoa huu, hivyo usilalamike fursa iko njoo uonyeshe ubunifu wako”.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, alisema ili kuendana na kasi ya maendeleo duniani inapasa kufanya mabadiliko makubwa ya sayansi na tekinolojia.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, alisema Bunge linatamani kuona bunifu zinazoibuliwa zinaboreshwa kwa dhana ya kuleta tija na kutatua kero mbalimbali za kijamii.