Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, ametoa wito kwa Watanzania kuepuka matumizi holela ya dawa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya ili kukabiliana na changamoto ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA).
Waziri Ummy alitoa tahadhari hiyo Juni 12, 2024, wakati wa mazungumzo maalum na Bwana Kido, Balozi wa Kampeni ya “Holela Holela Itakukosti” iliyozinduliwa kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutumia dawa kwa usahihi.
Katika hotuba yake, Waziri Ummy alisisitiza kuwa matumizi mabaya ya dawa husababisha athari nyingi, ikiwa ni pamoja na kuchelewesha kupona kwa mgonjwa, kuongezeka kwa magonjwa, na hatari ya kifo.
Alisema kuwa matumizi yasiyofaa ya dawa yanasababisha vimelea vya magonjwa kuwa sugu, hali inayowafanya wagonjwa kushindwa kutibika kwa urahisi
“Ni muhimu kuzingatia maelekezo ya madaktari unapopewa dawa. Hakikisha unamaliza dozi yote kama ilivyoelekezwa. Usitumie dawa ambazo ulitumia hapo awali au zilizotumiwa na mtu mwingine bila ushauri wa daktari,” alisema Waziri Ummy.
Aliongeza kuwa changamoto kubwa ni kutozingatia matumizi sahihi ya dawa. “Ukipewa dawa kwa siku saba, maliza siku zote saba, na kama ni 2×3, hakikisha unatumia ndani ya saa 24,” aliongeza. Waziri Ummy pia aliwataka wananchi kujiepusha kutumia dawa bila kupata ushauri wa kitaalamu, hasa dawa za antibiotiki
SomaZaidi;Watanzania Kufuata Ushauri wa Madaktari Matumizi ya Dawa
Serikali imechukua hatua zaidi kwa kuweka usimamizi wa maduka ya dawa chini ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) ili kuimarisha udhibiti wa usambazaji wa dawa na kupunguza tatizo la UVIDA. TMDA sasa ina jukumu la kuhakikisha kuwa dawa zinatolewa kwa kufuata cheti cha daktari na kusimamia matumizi sahihi ya dawa nchini
Katika kampeni ya “Holela Holela Itakukosti,” ambayo inaratibiwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Afya na mashirika mbalimbali, Waziri Ummy aliwahimiza wahudumu wa afya, wakiwemo madaktari na wafamasia, kuzingatia kanuni za utoaji dawa ili kuhakikisha Watanzania wanapata uelewa sahihi juu ya matumizi ya dawa
Waziri Ummy alisisitiza kwamba Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya matumizi holela ya dawa na umuhimu wa kutunza mazingira ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa sugu.
Kwa kuzingatia haya, ni wazi kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kukabiliana na tatizo la UVIDA na kuhakikisha afya bora kwa wananchi wote. Serikali, wataalamu wa afya, na wananchi kwa ujumla wanapaswa kushirikiana ili kutatua changamoto hii kwa manufaa ya jamii nzima.