Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Jerry Silaa, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika ziara ya kikazi nchini Rwanda, alipotembelea Wizara ya Mazingira yenye dhamana ya ardhi nchini humo.
Ziara hiyo ililenga kujifunza na kuona hatua zilizopigwa na Rwanda katika utekelezaji wa mfumo wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwenye usimamizi wa ardhi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Silaa alifuatana na Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara ya Ardhi, Bw. Fratern Hassan, na Balozi wa Tanzania nchini Rwanda, Mhe. Major Gen Ramson Mwaisaka. Walipokelewa na Waziri wa Nchi wa Rwanda, Mhe. Dkt. Claudine Uwera, aliyetoa maelezo ya kina kuhusu maendeleo makubwa yaliyofikiwa na nchi yake tangu mwaka 2004.
Mhe. Dkt. Uwera alieleza jinsi Rwanda ilivyoboresha mfumo wake wa usimamizi wa ardhi, ikitoka katika hali ya kutokuwa na sera wala sheria za ardhi na kuwa na hati za umiliki za kidigitali chini ya 1%. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 87 ya ardhi yote nchini Rwanda imepimwa na hati milioni 1.7 za kidigitali zimetolewa. Alisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada kubwa na uwekezaji katika TEHAMA.
Aidha, Mhe. Dkt. Uwera alikiri kwamba, pamoja na mafanikio ya Rwanda, mipango ya Serikali ya Tanzania ya kuwa na mfumo unganishi wa ardhi ni jambo la kujifunza. Aliipongeza Tanzania kwa hatua inayochukua kuelekea katika usimamizi bora wa ardhi kwa kutumia teknolojia.
ReadMore;Wanafunzi 700 Kusomeshwa Bure Na Serikali
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ardhi ya Rwanda (RNLA), Bibi Grace, alielezea jinsi mamlaka hiyo inavyoshirikiana na kamati za wananchi, maafisa mipango miji, na wapima wa kienyeji (parasurveyors) kupanga na kupima ardhi vijijini. Alifafanua kuwa ushirikishwaji wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha ardhi inapimwa na kusajiliwa kwa usahihi na uwazi.
Waziri Silaa alionyesha kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa na Rwanda na alisisitiza umuhimu wa Tanzania kujifunza kutoka kwa majirani zao. Alieleza kuwa, ushirikiano na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga na kupima ardhi ni jambo la msingi na linaendana na maagizo yake kwa wataalam wa ardhi nchini Tanzania.
Ziara hiyo imekuja wakati ambapo Tanzania inajadiliana kuhusu kuanzisha mamlaka ya usimamizi wa ardhi kama ilivyo RNLA ya Rwanda. Waziri Silaa alibainisha kuwa ziara hiyo itasaidia katika kuboresha na kuharakisha mchakato wa kuanzisha mamlaka hiyo nchini Tanzania.
ziara ya Waziri Silaa nchini Rwanda imekuwa ya mafanikio na kutoa mafunzo muhimu kwa Tanzania katika juhudi zake za kuboresha usimamizi wa ardhi kwa kutumia teknolojia na ushirikishwaji wa wananchi.