Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff wakati akielezea mafanikio ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Seff alisema kwamba yapo mengi yaliyofanyika na Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka mitatu hususan upande wa barabara.
Alisema barabara za vijijini ni muhimu sana kwani asilimia 65.1 ya watanzania wanaishi vijijini na shughuli zao kubwa hutegemea kilimo hivyo Serikali imeona umuhimu huo kwa kuongeza bajeti ya barabara na kuweza kutengeneza barabara maeneo ya vijijini.
“Serikali inatoa umuhimu kwa barabara za vijijini ikiwemo kuongeza bajeti mara tatu ukilinganisha na miaka ya nyuma na kufanya maeneo mengi kufikika”, aliongeza.
Aidha, Mhandisi Seff alitaja mkakati wa TARURA ifikapo mwaka 2025/2026 ni kufikisha asilimia 85 ya barabara zilizo korofi kupitika bila shida yoyote.
“Asilimia 69.1 ya barabara zilizobaki ni udongo na hivyo huathiriwa na mvua zinaponyesha na kufanya maeneo mengi kutopitika ila mkakati wetu hadi kufika mwaka 2025/2026 asilimia 85 zitakuwa zinafikika bila shida”.
Naye, Kaimu Mratibu wa kikosi kazi kinachosimamia miradi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia, Mhandisi Nyariri Nanai alisema TARURA imeshasaini mradi wa DMDP-2 na hivyo utekelezaji wake utaifanya Dar es Salaam kuondokana na mafuriko kwani mradi utajenga Km. 90 za mifereji ya maji na awamu hiyo ya pili itatekelezwa katika halmashauri zote tano.
Wakati huo huo Meneja wa TARURA mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga alisema Mhe. Rais ameongeza bajeti ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwa mkoa wa Dar es Salaam kutoka bilioni 20 hadi kufikisha bilioni 49 na hivyo kufanikiwa kuongeza kutengeneza sehemu kubwa ya barabara za jiji ambazo hapo awali zilikuwa zikiwasumbua wananchi.