Wataalam kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) wametakiwa kuandaa mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazokabili sekta ya posta.
Wito huu umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk. Mzee Suleiman Mndewa, wakati wa ufunguzi wa Vikao vya Kamati za Wataalam wa PAPU vilivyofanyika leo, tarehe 03 Juni 2024, jijini Arusha, Makao Makuu ya PAPU.
Dk. Mndewa alisema kwamba kila mmoja anafahamu changamoto zinazoikabili sekta ya posta, zikiwemo zinazowakumba waendeshaji wa huduma za posta na wateja. Hata hivyo, alionyesha matumaini kwamba utaalamu wa wajumbe wa mkutano huo utawezesha kutatua changamoto hizo.
Alisisitiza kwamba matumizi ya teknolojia ya kidijitali siyo hiari tena bali ni lazima kwa sekta ya posta, ili kuongeza ufanisi, uwazi, na ufikiwaji wa huduma za posta, hivyo kupunguza gharama na kuibua huduma mpya za kibunifu.
“Matumizi ya dijitali ni lazima kwa sekta ya posta ili kuongeza ufanisi, uwazi, na ufikiwaji wa huduma za posta, hivyo kupunguza gharama na kuibua huduma mpya za kibunifu,” alisisitiza Dk. Mndewa. “Tunayo matumaini ya kutosha kwa uwezo wenu mkiwa wataalam, kuzishinda changamoto hizo na kusaidia kuibuka washindi,” aliongeza.
SomaZaidi;Serikali Yatoa Onyo Kali Waajiri Wanaokwepa Michango NSSF
Amesema kamati za wataalam ni kiungo muhimu katika muundo wa PAPU, zikiwa na jukumu la kuendeleza, kuimarisha, na kukuza sekta ya posta katika Bara la Afrika. Kupitia kamati hizo, wataalam wanaibua fursa na masuala muhimu katika bidhaa na huduma za posta.
Kwa upande wa Tanzania, Dk. Mndewa alisema Posta inawajibika kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata huduma muhimu za posta.
Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mwakilishi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Salome Kessy aliwakaribisha nchini wageni kutoka nchi wanachama wa PAPU na kuwataka kutumia fursa ya uwepo wao nchini kutembelea vivutio vya utalii.