Wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Mazingira Duniani imeelezwa kuwa asilimia 20 ya samaki Ziwa Victoria wana chembechembe za plastiki kutokana na ongezeko la uchafuzi wa taka hizo ndani ya Ziwa hilo linalohudumia watu zaidi ya milioni 40.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Synergistic Globe Vitus Medard na kuitaka jamii kujiepusha na utupaji wa taka hususani pembezoni mwa Ziwa Victoria ili kulinda mazalia ya samaki katika ziwa hilo.
Soma Zaidi:Mawaziri Afrika Mashariki Wajadili Ukuzaji Viumbe Maji
Ameelezwa hayo hii leo na wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taka uliofanyika katika kata ya Luchelele jijini Mwanza ambapo amesema takwimu hizo ni kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa hivi karibuni na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) katika Ziwa Victoria na kubaini kuwa kati ya samaki watano mmoja ana chembe za plastiki.
Amesema katika jamii bado kumekua na baadhi ya wananchi ambao wanatupa uchafu pembezoni mwa ziwa Victoria na ndani ya Ziwa hali ambayo inahatarisha usalama wa samaki na mazalia ya viumbe hai ndani ya Ziwa hilo.
Amesema ili kupunguza uchafu katika ziwa hilo shirika hilo tayari limeanzisha mradi unaojulikana kwa jina la Marafiki wa Ziwa Victoria ukiwa na lengo la kusimamia, kuelimisha pamoja na kuhimiza uhifadhi wa vyanzo vya maji.
Amesema miongoni mwa vyanzo hivyo ni pamoja na vile vinavyotiririsha maji yake katika ziwa Viktoria lengo kubwa likiwa ni kutokomeza uchafu wa taka ngumu hususani plastiki ndani ya ziwa.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (MWAUWASA) Imrani Swai amelipongeza shirika hilo la Synergistic Globe kwa kazi kubwa ambazo linafanya na ameliomba liendelee kufanya kazi hiyo ili kuondoa uchafu ambao upo katika jamii.
Mratibu wa mradi wa marafiki wa ziwa Victoria Tabu Manyama amesema amesema kila mwananchi anayo jukumu la kutunza mazingira yote yanayomzunguka ili mazingira hayo yawe endelevu kwa jamii ya sasa na vizazi vinavyokuja hapo baadae.