Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Mkoa wa Arusha SACP Justine Masejo amepokea kompyuta pamoja viti ambavyo vitatumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa huduma za usalama kidigitali.
Aidha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Masejo ameishukuru Benki NMB kwa msaada huo, amesema vifaa vilivyotolewa vitakuwa msaada Mkubwa katika kutoa huduma bora na za kisasa kwa Wananchi.
Kamanda Masejo ameongeza kuwa vifaa hivyo vitaongeza ufasini katika utendaji wa kazi wa Jeshi hilo ikizingatiwa kuwa Mkoa huo unaendelea na mradi wake wakufunga kamera za kisasa katika Mitaa mbalimbali kwa ajili ya kuimarisha usalama wa Jiji hilo.
“Kwa vifaa hivi tunaimani vitaenda kutusaidia katika utendaji kazi wa kisasa, hata viongozi wetu wanasisitiza hilo kila siku hivyo niwashukuru sana NMB kwa kutuletea vifaa hivi”
Kwa upande wake Meneja wa benki ya NMB tawi la Clock Tower Arusha Bw. Praygod Mphuru amesema kuwa wametoa vifaa hivyo kuunga juhudi kubwa za Jeshi la Polisi za kuhakikisha Wananchi Mkoani humo wanakuwa salama.
Katika kuhakikisha Jeshi la Polisi linatoa huduma kidijitali, Benki ya NMB imeunga mkono Kwa kutoa vifaa mbalimbali ambavyo vitasaidia utendaji kazi wa haraka na bora.