Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na serikali ya Tanzania, leo zimeungana kuzindua kampeni ya “Holela- Holela Itakukosti” ambayo inaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Kampeni hii inazingatia udhibiti kuhusu usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA) na magonjwa ya kipaumbele ya zuonotiki (magonjwa ambayo yanaweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu).
Kampeni hii inaonyesha umuhimu wa kuchukua hatua za kuzuia na kudhibiti usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA) na magonjwa ya kipaumbele ya zuonotiki kuanzia katika ngazi za chini kwenye jamii kwa kutoa elimu na hatua za kuzuia maambukizi.
Soma Zaidi:Children With Epilepsy Excluded From National Health Insurance
Baadhi ya tabia hatarishi na uelewa mdogo wa kiafya na kisayansi miongoni mwa jamii nchini Tanzania unaifanya nchi kuwa katika hatari ya milipuko wa magonjwa ya kuambukiza. Kampeni hii itaziba mianya ya maarifa na kutoa mifano ya kile ambacho jamii inaweza kufanya ili kupunguza kuenea kwa magonjwa au kuugua.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo; Naibu Waziri ya Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema kwa kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko ya tabia, Tanzania inaweza kupunguza athari zinazotokana na udhibiti kuhusu usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA) na magonjwa ya kipaumbele ya zuonotiki (magonjwa ambayo yanaweza kuambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa wanadamu).
“Magonjwa yanayosababishwa na wanyama huambukizwa kati ya wanyama na wanadamu na ni hatari kwa kuwa yanaweza kusababisha milipuko na magonjwa ya kuambukiza. Ni muhimu kuzingatia, kutambua, kudhibiti, na hatimaye kuondoa magonjwa haya ili kuhakikisha jamii na wanyama wanabaki wenye afya na kuepuka matatizo ya kiuchumi na kijamii. Kampeni ya ‘Holela-Holela Itakukosti’ ni mfano mmoja wa jinsi USAID inavyofanya kazi katika jamii kuboresha na kudumisha afya na ustawi wa wote.” Amesema Dkt. Mollel.