Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu amesema mchango wa kumnunulia gari umefika Sh. milioni 20 ndani ya siku tano tangu kuanza kwa harambee hiyo.
Kupitia video fupi aliyoiweka jana kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X, Lissu alisema ameshapokea Sh. milioni 20 sawa na wastani wa Sh. milioni nne kwa siku.
Alishukuru Watanzania kwa kumchangia kiasi hicho cha fedha na kuwaomba kuendelea kuchangia ili kufikia malengo ya kununua gari jipya ili lile la zamani liwekwe Makumbusho ya Taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo kujifunza.
Soma Zaidi:Lissu Raises The Controversy Of The rising Sugar Prices.
Lissu alieleza kuwa watu waliomchangia fedha hizo mpaka jana wakati anatoa taarifa ni 1,673 sawa na wastani wa Sh. 12,000 kwa kila mchangiaji.
“Ninawaomba kuendelea kuchangia kwa kiasi chochote mlichonacho ili gari lipatikane na kazi ya ukombozi wa wananchi iendelee.
“Elfu moja yako, Sh. 10 yako au kiasi chochote ulichonacho kitatuwezesha kufanya kazi kubwa ya ukombozi wa umma ambao unahitajika,” Lissu alisema.
Wiki iliyopita Lissu alikabidhiwa gari lake aina ya Toyota Land Cruizer V8, VXR na Jehi la Polisi mkoani Dodoma ikiwa imepita takriban miaka saba tangu liliposhikiliwa na jeshi hilo baada ya mwanasiasa huyo kushambuliwa kwa kupigwa risasi akiwa kwenye gari hilo na watu wasiojulikana, nyumbani kwake Area D, Septemba 7, 2017.
Baada ya kukabidhiwa gari hiyo, Lissu alisema atalitengeneza ili aendee kulitumia katika shughuli zake za kisiasa mpaka pale litakapochoka, lakini wafuasi wake walisema watamchangia fedha za kununua gari lingine ili hilo liwe ukumbusho juu ya kile kilichomsibu.
Mwanaharakati Maria Sarungi ndiye aliyeanzisha harambee ya kumchangia fedha Lissu ili anunue gari lingine. Kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram na X. Maria aliweka tangazo linalosomeka: “Tumchangie Tundu Lissu anunue gari jipya,” akiambatanisha namba za kupokea fedha.
Hoja hiyo iliungwa mkono na watu mbalimbali akiwamo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob aliyeahidi kuchangia Sh. milioni mbili ili kumwezesha kiongozi huyo kununua gari na Godbless Lema aliyeandika ujumbe wa kuhamasisha kwenye ukurasa wake wa mtandao wa X.