Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha imetoa elimu kwawalimu wa Shule za Msingi, Sekondari na Wakuu wa Idara za Elimu na kuwaelimisha kuhusu masuala ya fedha ikiwemo kujiepusha na mikopo isiyo salama.
Semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa St. Clara, wilayani Biharamulo mkoani Kagera, ambapo zaidi ya walimu 650 wameshiriki semina hiyo ambapo walipata fursa ya kujifunza mada zaidi ya nne ikiwemo, kujiwekea akiba, mikopo, uwekezaji, na usimamizi wa fedha binafsi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti washiriki wa semina hiyo akiwemo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mizani Bi. Ephransia Zakayo, alisema kuwa kupitia semina hiyo amejifunza kuwa kabla ya kuchukua mkopo ni lazima mkopaji aainishe malengo ya kuchukua mkopo huo lakini pia matumizi ya mkopo na namna alivyojipanga kurejesha ili asiingie kwenye migogoro.
“Kupitia elimu hii nimejifunza pia umuhimu wa kuwa na vipaumbele katika maisha yetu ya kawaida, ukiwa na vipaumbele itakusaidia kutokua na tamaa na itasaidia kutokukupeleka kwenye mikopo ambayo hukupanga kuchukua”, alisema Bi. Zakayo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kikomakoma, Bw. Lukanga Yassin, ameishukuru Serikali kwa kuwafikia na kuwapa elimu ambayo imewapa uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwemo kuwa na matumizi sahihi na kuweka akiba wanapopata fedha sio kuzitumia zote.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa kumekua na mwitikio mkubwa kwa walimu na wameonesha nia ya kufanya uwekezaji katika Taasisi mbalimbali rasmi.
Soma Zaidi:Watoa Huduma za Fedha Waonywa kwa Kuvunja Sheria
“Katika makundi mbalimbali tuliyowafikia Wananchi wameahidi kubadilisha mtindo wa maisha ikiwemo kuacha kukopa kwa mazoea, lakini pia kuanza utaratibu wa kusoma mikataba kabla ya kusaini ili kupunguza kama sio kumaliza kabisa migogoro ya mikopo” alisema Bw. Kibakaya.
Kwa kutambua umuhimu wa elimu ndogo ya fedha kwa wananchi wa Tanzania mwaka 2021, Serikali kupitia Wizara ya Fedha ilianzisha rasmi Wiki ya Huduma Ndogo za Fedha ambayo hufanyika kila mwaka, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha katika ngazi zote za Mjini na Vijijini.
Kwa sasa Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TAMISEMI na Taasisi nyingine za Serikali, imemaliza zoezi la utoaji elimu ya huduma ndogo za fedha kwa Wananchi wa Mikoa ya Kagera, Singida na Manyara.
Sasa ni zamu ya wananchi wa mikoa ya Rukwa na Kigoma kuweza kufikiwa na kupatiwa elimu ya huduma ndogo za fedha ili waweze kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.