Serikali imesema kuwa mwaka 2017 kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa biashara, ilitoa mwongozo wa pamoja wenye dhima ya kuunganisha tozo na kodi mbalimbali kwa nia ya kupunguza wingi wa tozo na kodi ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.
Hayo yameelezwa bungeni, jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Mpendae, Mhe. Toufiq Salim Turky, aliyeuliza Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kunakuwa na muunganiko wa kodi ili kupunguza utitiri wa kodi usio wa lazima kwa wawekezaji.
Soma zaidi:Serikali Yaondoa Tozo Gesi ya Magari
Mhe. Chande alisema kuwa mpango huu umekuwa ukitekelezwa kwa ufanisi mkubwa kupitia marekebisho mbalimbali ya Sheria ya Fedha, kuanzia mwaka 2018 hadi 2023, kwa kupunguza na kuondoa kodi na tozo mbalimbali.
‘‘Serikali itaendelea kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa na wadau yanakamilishwa kama yalivyopangwa ili kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini,’’ alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande alifafanua kuwa mwelekeo wa Serikali ni kuifanya mifumo yote iwe pamoja ili kupunguza wingi wa kodi, tozo na usumbufu kwa wafanyabiashara na kuwa mifumo hiyo itakapokamilika taarifa itatolewa kwa umma.