Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, ametoa wito kwa waandishi wa habari kuwa na uelewa mzuri wa michakato ya Bunge ili kuripoti kwa usahihi na kuepusha kuzua taharuki kwa wananchi.
Waziri Nnauye amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa na utaalam maalum katika kuripoti shughuli za Bunge na sekta nyingine muhimu kama uchumi, sheria, na afya.
Katika mkutano uliofanyika jijini Dodoma, Waziri Nnauye alieleza kuwa mazungumzo yamefanyika kati ya wizara yake na Bunge kwa lengo la kubuni mpango maalum wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu namna bora ya kuripoti shughuli za Bunge. “Tumeshauriana na Bunge kama mnataka shughuli zenu ziripotiwe vizuri, tutengeneza utaratibu wa kuwafunza watu wajue,” alisema Nnauye. “Kama wizara tuta-push hili tupate waandishi, kwanza wa specialize shughuli za ripoti za Bunge, kila siku akija mpya atapotea tu.”
Waziri Nnauye alibainisha kuwa wizara yake itaweka mkazo katika kuwawezesha waandishi wa habari kuwa wabobezi katika maeneo maalum kupitia mpango wa Bodi ya Ithibati ambayo inatarajiwa kusaidia kuleta ubora zaidi katika ripoti za habari. Alisema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kuwa na utaalam wa ndani katika sekta wanazoripoti ili kuhakikisha taarifa zinazotolewa ni za uhakika na zinaelimisha umma vizuri.
Mbali na kuimarisha ubora wa ripoti za Bunge, Nnauye alitoa taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali kuimarisha sekta ya habari nchini. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2023/2024, kumekuwa na ongezeko la idadi ya vituo vya televisheni kutoka 65 mwaka 2023 hadi 68 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 4.6. Vile vile, idadi ya vituo vya kurusha matangazo ya redio imeongezeka kutoka vituo 215 mwaka 2023 hadi kufikia vituo 231 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 7.4
SomaZaidi;Waandishi wa Habari: Ubunifu Duni na Tabia ya Kuiga
Kwa upande wa magazeti, idadi imeongezeka kutoka 321 mwaka 2023 na kufikia 351 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 9.3. Waziri Nnauye alisema kuwa ongezeko hili limechangiwa na serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za utangazaji, hasa maudhui mtandaoni, hali ambayo pia imeongeza ajira kwa vijana waliojikita katika sekta hiyo
Nnauye pia alizungumzia kuhusu uhuru wa vyombo vya habari nchini na kusema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kulinda uhuru huo, ikishika nafasi ya kwanza Afrika Mashariki na nafasi ya 97 kimataifa kwa mujibu wa World Press Freedom Index 2024, ikilinganishwa na nafasi ya 143 mwaka 2023. Alisema kuwa hatua hizi zimewezekana kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na serikali ikiwemo Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2023
Waziri Nnauye alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kufuata maadili na kuwa na ujuzi maalum wa kuripoti shughuli za Bunge. Alisema, “Bodi ya Ithibati itasaidia kuwawezesha waandishi kuwa wabobezi.” Hii ni sehemu ya mkakati wa wizara kuhakikisha kuwa sekta ya habari inakua na mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kwa kutoa taarifa sahihi na za kuaminika kwa umma.
you have a great blog here! would you like to make some invite posts on my blog?