Katika juhudi za kuimarisha usalama na kulinda haki za binadamu, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Fabian Mhagale amewataka wananchi wa Kata ya Mvungwe, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Mhagale alisisitiza umuhimu wa ushirikiano huo hasa katika kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino, ambao mara nyingi wamekuwa wakilengwa na wahalifu kwa sababu ya imani potofu na ushirikina.
Mhagale alisisitiza kuwa uongozi wa kata hiyo unashirikiana na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kuhakikisha usalama wa watu wenye ualbino. Amewaomba wananchi kutoa taarifa za watu wanaofanya ukatili au wenye mipango ya kufanya ukatili dhidi ya albino, akibainisha kuwa ulinzi umeimarishwa kufuatia matukio ya hivi karibuni ya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino katika mikoa ya Kagera na Geita.
SomaZaidi;Ukatili Dhidi Ya Albino walaaniwa Vikali
Wakati akitembelea familia moja yenye watu wenye ualbino katika kata hiyo, Mhagale aliihakikishia familia hiyo kuwa iko salama na kuwataka kutoa taarifa haraka pale watakapokuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao. Alisema, “Wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu vitendo vyovyote vya uhalifu au mipango ya uhalifu ili kusaidia kuwalinda wale walio hatarini, hasa watu wenye ualbino.”
Aidha, Mhagale alizungumzia hatua za kuimarisha ulinzi kwa kushirikiana na wananchi ili kuzuia matukio ya ukatili, akisisitiza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na polisi ni muhimu katika kutokomeza uhalifu na kuhakikisha usalama wa jamii.
Mkoa wa Tanga umekuwa ukikabiliwa na changamoto mbalimbali za kiusalama, ikiwemo vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ualbino. Hivyo, juhudi za Jeshi la Polisi kushirikiana na jamii ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hizi na kuimarisha usalama wa wananchi wote.