Maandalizi makubwa yanaendelea jijini Arusha kwa ajili ya Mkutano wa Kawaida wa 45 wa Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambao utaanza tarehe 28 Juni, 2024.
Mkutano huo, ambao unafanyika chini ya uwenyeji wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, utahudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu na wajumbe kutoka nchi wanachama zote, ikiwa ni pamoja na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na Somalia ambayo itashiriki kwa njia ya mtandao.
Maandalizi ya mkutano huu muhimu yalianza na Kikao cha Maafisa Waandamizi tarehe 22 Juni, 2024, ambacho kinamalizika leo tarehe 24 Juni, 2024. Baada ya kikao hicho, Makatibu Wakuu watashiriki katika vikao kuanzia tarehe 25 hadi 27 Juni, 2024, kwa lengo la kuhitimisha mazungumzo ya maandalizi kabla ya Mkutano wa Mawaziri.
Ajenda kuu kwa Mawaziri ni pamoja na kupitia utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika mikutano ya awali, kujadili masuala ya forodha na biashara, na kupitia ripoti za miundombinu, sekta za uzalishaji, masuala ya kijamii, na maendeleo ya kisiasa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
SomaZaidi;Urusi na China: Kususia Mkutano wa Amani wa Uswisi
Kwa kuongezea, taarifa kutoka kamati mbalimbali zinazohusika na fedha, rasilimali watu, na taarifa za mkutano wa Makatibu Wakuu uliofanyika tarehe 17 Mei, 2024, zitawasilishwa. Aidha, kalenda ya matukio yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Julai hadi Desemba 2024 ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki itajadiliwa pia.
Mkutano huu wa 45 wa Baraza la Mawaziri unathibitisha azma ya nchi wanachama wa EAC katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na maendeleo ya pamoja katika maeneo mbalimbali, lengo likiwa ni kukuza uchumi, maendeleo ya kijamii, na utulivu wa kisiasa katika eneo hili la Afrika Mashariki.